Genesis 4

Kaini Na Habili

1 aAdamu akakutana kimwili na mkewe Hawa, naye akapata mimba, akamzaa Kaini. Hawa akasema, “Kwa msaada wa Bwana nimemzaa mwanaume.” 2 bBaadaye akamzaa Habili ndugu yake.

Basi Habili akawa mfugaji, na Kaini akawa mkulima.
3 cBaada ya muda Kaini akaleta baadhi ya mazao ya shamba kama sadaka kwa Bwana. 4 dLakini Habili akaleta fungu nono kutoka baadhi ya wazaliwa wa kwanza wa mifugo yake. Bwana akamkubali Habili pamoja na sadaka yake, 5lakini Mungu hakumkubali Kaini pamoja na sadaka yake. Kwa hiyo Kaini akakasirika sana, uso wake ukawa na huzuni.

6Kisha Bwana akamwambia Kaini, “Kwa nini umekasirika? Kwa nini uso wako una huzuni? 7 eUkifanya lililo sawa, je, hutakubalika? Lakini usipofanya lililo sawa, dhambi inakuvizia mlangoni mwako, inakutamani wewe, lakini inakupasa uishinde.”

8 fBasi Kaini akamwambia ndugu yake Habili, “Twende shambani.” Walipokuwa shambani, Kaini akamshambulia Habili ndugu yake, akamuua.

9 gKisha Bwana akamuuliza Kaini, “Ndugu yako Habili yuko wapi?”

Akamjibu, “Sijui, je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?”

10 h Bwana akasema, “Umefanya nini? Sikiliza! Damu ya ndugu yako inanililia mimi kutoka ardhini. 11 iSasa umelaaniwa na umehamishwa kutoka ardhi, ambayo imefungua kinywa chake na kupokea damu ya ndugu yako kutoka mkononi mwako. 12 jUtakapoilima ardhi, haitakupa tena mazao yake. Utakuwa mtu wa kutangatanga duniani asiye na utulivu.”

13Kaini akamwambia Bwana, “Adhabu yangu ni zaidi ya niwezavyo kustahimili. 14 kLeo unanifukuza kutoka nchi, nami nitafichwa mbali na uwepo wako. Nitakuwa mtu wa kutangatanga asiyetulia duniani na yeyote anionaye ataniua.”

15 lLakini Bwana akamwambia, “La sivyo, ikiwa mtu yeyote atamuua Kaini atalipizwa kisasi mara saba zaidi.” Kisha Bwana akamwekea Kaini alama ili mtu yeyote ambaye angemwona asimuue. 16 mKwa hiyo Kaini akaondoka mbele za Bwana akaenda kuishi katika nchi ya Nodi, iliyoko mashariki ya Edeni.

17 nKaini akakutana kimwili na mkewe, naye akapata mimba na akamzaa Idrisi. Wakati huo Kaini alikuwa anajenga mji, akauita Idrisi jina la mtoto wake. 18Idrisi akamzaa Iradi, Iradi akamzaa Mehuyaeli, Mehuyaeli akamzaa Methushaeli, na Methushaeli akamzaa Lameki.

19 oLameki alioa wanawake wawili, mmoja aliitwa Ada, na mwingine Sila. 20Ada akamzaa Yabali ambaye ni baba wa wale walioishi katika mahema na kufuga wanyama. 21 pKaka yake aliitwa Yubali, aliyekuwa baba wa wote wapigao zeze na filimbi. 22 qPia Sila alikuwa na mtoto wa kiume aliyeitwa Tubali-Kaini ambaye alifua vifaa vya aina mbalimbali vya shaba na chuma. Naama alikuwa dada wa Tubali-Kaini.

23 rLameki akawaambia wake zake, “Ada na Sila nisikilizeni mimi;
wake wa Lameki sikieni maneno yangu.
Nimemuua mtu kwa kunijeruhi,
kijana mdogo kwa kuniumiza.

24 sKama Kaini atalipizwa kisasi mara saba,
basi Lameki itakuwa mara sabini na saba.”

25 tAdamu akakutana kimwili na mke wake tena, akamzaa mwana, akamwita Sethi, akisema, “Mungu amenijalia mwana mwingine badala ya Habili, kwa kuwa Kaini alimuua.” 26 uNaye Sethi akamzaa mwana, akamwita Enoshi.

Wakati huo watu wakaanza kuliitia jina la Bwana.
Copyright information for SwhKC